Friday, May 29, 2020

WINNING IS ALL I DO

Assalamualaikum

      Leo naleta uzi utakaotembea kwa jina la WINNING IS ALL I DO hapa naelezea au kukuasa kutojihusisha na biashara ya wahuni wanajiita QNET, AIM GLOBAL pamoja na binamu zao. Hawa jamaa wamekuwa wakilaghai watu kwa kiwango kikubwa sana
       Ili nisikuchoshe mpendwa msomji wa ukurasa huu, twende chap chap kwenye uzi husika, iko hivi, hii biashara hujulikana kama e commerce yaaani electronic commerce, hii unanunua bidhaa mtandaoni yaani kwa internet
     Hawa jamaa wako na swagger zao fulani tamu sana,  utasikia ukiunganishwa na wewe ukaunganisha watu kadhaa unakuwa millionaire, leo nakuibia siri kama kweli unakuwa millionaire muone viatu vyake utakuta kanunuaga vile bibuti vya jeje na soli imeisha upande, jiulize yeye mbona hajawa millionaire?

  Watumishi wengi wa serikali hasa Sekta ya elimu(hapa nawazungumzia walimu wenzangu) wamekuwa wahanga wakubwa wa janga hili, yaani unakuta ka risk kama 1m hadi 4m huku akitarajia kuwa future millionaire na wanapenda kunifariji kwa kuitana ama wanapopeana hi utasikia Good morning millionaire
  
Pamoja na kuitana majina matamu yanayo sound vizuri, watu hawa ndo wanaongoza kwa mizinga kuliko hata Girl friend wako utasikia una buku hapo!

  Ukweli uko hivi, ukisha kuunganishwa na kutoa pesa ya kiingilio unatakiwa uunganishe watu almost 16 hii ni kama kuchanganua sentensi kwa njia ya matawi, walimu wenzangu wa kiswahili nafikiri hapa mnanielewa vilivyo, utakuta mtu anamiaka karibia 6 hadi 7 toka aunganishwe hajaunga hata mmoja au kaunga watatu na tayari ashajua kuwa aliingia mkenge lakini haachi kutafuta watu ili awachomeshe nao, hawa QNET, AIM GLOBAL, SIJUI ALLIANCE hawana tofauti na BAY PORT
Ukiwaona usiwasikilize, nakwambia usiwape nafasi ya kuwasikiliza kama F3 Response yako ni freeze mode umeisha mimi yangu ni fight mode hawaniwezi hata wakiungana

Friday, May 15, 2020

UNAMFAHAMU MZEE WA MSOGA

Mfahamu Dr. Jakaya Kikwete: Mzee wa za Kuambiwa Changanya na za Kwako!

Denis Mpagaze
____________________________

Mzee Kikwete alizaliwa Oktoba 7, 1950 katika kijiji cha Msoga, Pwani katika familia ya watoto tisa, akasoma msingi hadi chuo kikuu, akatumikia jeshi na chama kwa bidii na uadilifu akavuna ubunge, uwaziri na urais, akaendesha nchi kwa uhuru wa kila mtu kujiachia, tukamlipa matusi na kejeli, siku anaondoka akasema mlisema mimi ni mpole sasa nawaletea mkali, akatukabidhi kwa John Pombe Magufuli, Mzee wa mimi sijaribiwi, kisha akurudi zake Msoga vilio vya kummiss Jakaya vikaanza kusikika kila kona ya nchi mithili ya wana wa Israel walivyomtukana Musa awarudishe Misri, wahenga tukasema, “Hakuna jipya chini ya Jua!”

Lakini tuache masihara aisee, enzi za Mkwere watu walikula bana. Unakumbuka habari za laki si pesa? Shilingi mia kuitwa jiti je? Nchi ilikuwa full shangwe, ponda mali ukifa usijute, aliyekopesha alisahau kudai, wenye vyeti feki walipata heshima na maandamano ya kisiasa yalikuwa bureee kabisa, wapinzani walitafuna vya ikulu bila kujali itikadi, vijana wakasumbua huko baa na klab kwa lete kama tulivyo, keep change ikawa habari ya mujini, walimu nao wakaibuka na kibwagizo cha "shemeji unatuachaje". Watu walitafuna hadi mabilioni ya Kikwete bila huruma kama wabunge wa Uganda kula hela za corona. Shame!

Shibe ilipozidi tukamuita Jakaya dhaifu, Vasco Dagama, muhuni kwa sababu too much of anything is harmful.Tatizo ukishiba sana lazima urukwe na akili, usiposhiba kabisa unakuwa tapeli. Maisha huwa siyaelewi kabisa.

Tatizo Jakaya aliruhusu demokrasia hadi pasipohitaji demokrasia. Hivi uandeal vipi na mafisadi kwa kuwaambia wajishughulikie??? Au umesahau enzi za kujivua gamba, kampeni iliyoshupaliwa na Nape Mnauye utadhani yeye ndo alikuwa CCM zaidi ya Nyerere. Mie nilikuwa nampimia tu. Enzi hizo Nape akikohoa chama kinapiga chafya, siku hizi cheee. Kweli kila zama na kitabu chake. Kwa mara ya mwisho nilimuona Nape Ikulu akiomba msamaha kwa baba yake baada ya kunaswa na ndoano ya mvuvi. Ila Nape bwana. Yeye si ndo alitufundisha kwamba samaki anayefumbua mdomo ndo hunaswa na ndoano? Sasa ilikuaje akanaswa yeye?  Au ndo yale mahubiri ya sikiliza maneno yangu usifuate matendo yangu amina.Ajabu kweli.

Siku moja baada ya kukamilika kwa siku 90 za kujivua gamba, Rostam Azizi aling’atuka tukasema ni gamba kumbe mshikajia aliamua kuachana na siasa za maji taka nakwenda zake kwenye biashara, akarudi kutusaidia wakati wa janga la covid-19.  Rostam ndo katuletea mashine ya kupima virusi vya corona Zanzibar. Barikiwa sana mwanangu Rostam Azizi popote ulipo.

Halafu Rostam Azizi bana, alipoulizwa mashine hiyo imegharimu kiasi gani akasema yeye hajui, wanajua vijana wake wa mambo ya fedha, yeye anachojua mashine imenunuliwa. Ukiwa na pesa bana, huna muda wa kuwakaba kabale wafanyakazi wako kama mchunga mbwa. Wahasibu wa shule na vyo vya private wanavyo henya!

Unajua nimekuwa nikijiuliza kwa nini Jakaya alikuwa mtu wa kuamini kila mtu hadi akaamini majizi yakampiga na wakati ShakeSpear aliwahi kusema penda wote, amini wachache. Nikagundua ni kwa sababu ya historia yake ndefu aliyopitia hadi kufika Ikulu. Kwanza alitoka katika familia ya kifalme,babu yake alikuwa mfalme wa Wakwere na baba yake DC kwahiyo hana historia ya kulala njaa kama baba yako. Babu yake ndo alimtabiria Kikwete mtoto wa sita kuzaliwa kuwa kiongozi mkubwa. Babu alifanya hivyo Jakaya akiwa tumboni kwa mama yake.

Utabiri wa babu ukatimia. Jakaya akiwa Kibaha Sekondari alikula uenyekiti wa wanafunzi na vijana wa TANU, Tanga sekondari akawa Kiranja Mkuu na chuo kikuu Mlimani  akawa mwenyekiti wa halmashauri ya wanafunzi. Mpaka hapo wengi katupiga chini maana hatujawahi kupata hata umonita. Sasa bro kama hata umonita hujapata halafu leo unachukua fomu kugombea huoni kama utaishia magereza?

Jakaya alitoka Mlimani mwaka 1975 na jiwe la uchumi na April 2, 1975 akalenda Singida kutumikia chama kisichokuwa na maslahi kwa nafasi ya Ukatibu Msaidizi wa TANU Mkoa wa Singida.Enzi hizo vyama vya siasa viliendeshwa kama vigango, no mishahara, full kupiga myayo. Usione mbwembwe za wanachama wa vyama vya siasa hakuna kitu pale. Watu wako vyamani kuzengea uteuzi tu.Povu ruksa!

Mwaka 1976 Jakaya aliingia Jeshini lakini CCM ilipozaliwa alipelekwa Zanzibar kukijenga chama. Alipiga kazi Zenj hadi mwaka 1980 alipopelekwa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Utawala, Idara ya Ulinzi na Usalama na Msaidizi wa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM enzi hizo Mzee Pius Msekwa. Haya maisha haya. Yaani Jakaya alitumwa na Msekwa, baadaye Msekwa akatumwa na Jakaya. Mwaka 1981 Jakaya alishushwa hadi kuwa Katibu Mtendaji wa CCM Mkoa wa Tabora. Jamaa akaenda huko bila kutia neno, akayashinda majaribu.

Kutoka Tabora mwaka 1983 alijiunga na Chuo Kikuu cha Maofisa wa Jeshi Monduli, akala Uluteni Kanali na kuwa Mkufunzi Mkuu na Kamisaa wa siasa katika chuo hicho. Kwa tabasamu la Jakaya huwezi amini kama alikuwa mjeshi, tena machachari. Kuna jamaa alitusimulia kisa cha Jakaya kutoka Monduli, nikashangaa sana. Sasa sijui jamaa alitufunga kamba?

Jamaa mwenyewe alisema Jakaya alimuandikia Rais Nyerere barua kumshitaki mkuu wa chuo Luteni Jenerali Gideon Fundi Sayore kwa kuchanganya biashara na ajira kinyume na sera za Ujamaa. Sayore alikuwa mfugaji na mkulima mkubwa aliyekiuzia chuo nyama, maziwa, maharage na mahindi. Nyerere baada ya kuisoma ile barua alimkabidhi Jenerali David Musuguli, mkuu wa majeshi enzi hizo akisema, “Hayo ni mambo yenu kayamalizeni hukohuko."

Sasa badala ya Msuguli kuchukua hatua, yeye akairudisha ile barua kwa Mzee Sayore, Sayore akafura, tukajua Jakaya anatafunwa. Sayor akaitisha kikao pale jeshini na kuanika barua ya Jakaya hadharani huku akigonga meza kwa hasira. Aivyotoka nje na kusema anarudi, Jakaya mtoto wa mujini, akala kona mazima, hakurudi tena jeshini. Alikula pori kwa pori, tena kwa mguu.

Njiani Jakaya alikutana na mwanajeshi mfupi kuliko wote, walimtania Pimbi wa Monduli,ni Balozi Abruhaman Shimbo. Jakaya akamsimulia yaliyomkuta, Shimbo akamuunganisha na mjomba wake wa Tengeru, Jakaya akapata pa kufikia, akapumzika siku kadhaa, akapewa nauli akarudi zake Bagamoyo.

Shimbo alitenda wema na kwenda zake, akakutana nao mbeleni siku Jakaya alivyokamata nchi.  Shimbo alikula unadhimu mkuu wa Jeshi la wananchi na baadaye balozi wa China. Watu wakachonga ati Jakaya anagawa vyeo kishikaji. Hivi hata ingekuwa wewe unaanzaje kumuacha mtu kama Pimbi wa Monduli? Tubutu!!!!

Kwa sababu Jakaya alikuwa hazina ya chama Mzee Kawawa aliamua kumpeleka kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea na mwaka 1988 akahamishiwa Wilaya ya Masasi. Kawawa alitisha.  Imagine mkufunzi wa chuo cha kijeshi, graduate na meja wa jeshi kupelekwa kufanya kazi za darasa la nane tena Lindi. Mzee Sinde Warioba wakati huo ni Waziri Mkuu ndo alimnyofoa huko na kumleta mujini na kumuombea ubunge kwa Mzee Mwinyi. Mwinyi akampa Jakaya shavu la ubunge wa Taifa na kisha unaibu waziri wa nishati na madini, mwaka 1990 akapandishwa cheo jeshini na kuwa Luteni Kanali kwa sababu aliyenacho huongezewa. Mwaka 1992 siasa ilivyofutwa jeshini, Jakaya alistaafu zake jeshi kwa hiari!

Mwaka 1995 Jakaya, Joseph Warioba, Mark Bomani, Cleopa Msuya, John Malecela, Edward Lowassa, Kighoma Ali Malima, Benjamin Mkapa, Horace Kolimba, Rose Lugendo, Pius Msekwa, Tuntemeke Sanga, Njelu Kasaka na Fred Rutakyamirwa wakatupa kete kwenye kiti cha urais akaibuka Mkapa. Kolimba na Malecela walikatwa mapema na mwalimu kwa sababu walishindwa kumsaidia Mwinyi. Nyerere aliishawachukia Kolimba na Malicela kitambo hadi kuwatungia kitabu cha “Hatima ya Tanzania na Uongozi Wetu.” Tafute ukisome kama huna pepo la kusoma vitabu. Maana kuna mtu akishika kutabu tu anasinzia.Hilo ni pepo la umaskini wa maarifa likemee!

Mchujo uliendelea hadi wakabaki watatu, Kikwete, Mkapa na Msuya. Kikwete aliongoza kwa kura 534 akifuatiwa na Mkapa aliyepata kura 459 na Msuya akafunga mkia kwa kura 336. Kwa kuwa kanuni inataka mshindi apate zaidi ya asilimia hamsini, Kikwete hakuwa mshindi. Ngoma ikarudiwa, Mkapa akaibuka kidedea kwa kura 686 na Kikwete kura 639, tonge la urais likamponyoka.

Jakaya akasubiri tena kwa miaka kumi kwa sababu mvumilivu hula mbivu, Kolimba akaponda ati CCM imepoteza dira, akatishia kuhamia upinzani, Profesa Malima akaona huu ni utoto, akahamia NRA, lakini mwaka huohuo alikufa ghafla, mwanaye Adam Malima akashika mikoba lakini baadaye alikuja kuwa waziri kwenye serikali ya Jakaya.

Adam Malima ndo yule jamaa aliyetis SMG na polisi na polisi machachari kwa risasi tatu hewani na halafu Adam hakushituka, alibaki kuwacheki, huku akitabasamu, jamaa yangu akaropoka, "huyu polisi atakuwa na vyeti feki." Nikamwambia ziba domo lako kabisa usijekupotezwa ukatusumbua kutunza watoto wako. Adam akapelekwa central na kupandishwa mahakamani halafu Magufuli akamteua Adam kuwa RC wa Mara. Wenye roho za visasi wakaanza, “Ningekuwa mimi ni Adam ningemuomba Siro amuhamishie yule polisi mkoa wangu alafu namuomba RPC anipe awe mlinzi nyumbani kwangu, mbona angeacha kazi mwenyewe”. Uzuri Malima si mtu wa visasi.

Tutemeke Sanga wa Makete naye akatishia kuunda chama chake. Huyu Tutemeke ndo yule jamaa aliyezinguana na Nyerere baada ya kutoka kusoma majuu na elimu kubwa alipoulizwa na mwalimu apewe kazi gania, akasema nataka urais, kimsingi alikosa adabu mbele ya mjamaa, akatiwa kizuizini, akapigwa njaa hadi mke wake wa kizungu akakimbia. Enzi za Nyerere ukijichanganya ulikwenda kizuizini, ukiiba ni jela na viboko juu ili ukirudiumuonyeshe mke wako.

Habari zikasambaa mitaani ati Nyerere alimkataa Jakaya kwa sababu alikuwa mdogo. Habari nyingine zikasema kilichomponza Jakaya ni uswahiba wake na Lowassa  maana walikwenda Dodoma kuchukua fomu dakika za mwisho kwa ndege ya kukodi. Nimetafuta maneno ya Nyerere aliyoyasema hadi sasa sijayapata. Nachojua kukatwa kwa jina la Lowassa kulileta mtikisiko mkubwa kama alivyosimulia Prof. Chachage Chachage mwandishi wa kitabu cha “Makuadi wa Soko Hurua.” Ule wa 2015 ulikuwa cha mtoto. Unaikumbuka ile single ya Tunaimani na Lowassa, oyaa, oyaa, oyaa! Alipokatwa imani za watu wake zikawa haba!

Kitu kikubwa alichokifanya Mkapa baada ya kuchukua Ikulu, ni kumpa Jakaya Uwaziri wa mambo ya nje kwa miaka 10, Jakaya akashikana mikono na dunia. Alikwenda hadi kwa Mandela kurudisha pea moja ya viatu alivyoviacha Tanzania enzi za harakati za uhuru! Mandela aliviacha kwa marehemu Nsilo Swai. Ilikuwa mwaka 1962. Walipofika Sauz, Mandela alimkumbatia Vicky mke wa Swai na kusema, “You are a good friend”, wakapiga picha! Mandela akampa zawadi ya kitabu na wakati mswahili ukimpa zawadi ya kitabu anakutukania moyoni, ukimpa zawadi ya hela anakubariki hadharani.Bure kabisa!   

Miaka kumi ya Mkapa ikaisha, Jakaya akarudi tena ulingoni, fomu wakachukua wengi, panga likapita, ulingoni wakabaki Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na Dr. Salim Ahmed Salim. Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku na vigogo wengine wakamsupport Salim na Jakaya akasapotiwa na Rostam Aziz na Comrade Edward Lowassa. Fitina zikachezwa, Salim akapigwa zengwe la uarabu na muuaji wa Karume, akababaika na kujitetea ati ni mnyamwezi, ila ana ndugu Oman, kura zikapigwa, Jakaya akashinda, Salim akakaa chini, Butiku akaduwaa na Warioba akashangaa!

Jakaya akachukua nchi kwa kishindo cha asilimia 81, historia ikaandikwa, wapinzani wakamkamata Mchina uchawi kwa kutengeneza karatasi zenye vema ya kutegeshea Jakaya ashinde kwa sababu Afrika hakunaga kushindwa, huwa kuna kushinda na kuibiwa tu.

Jakaya akaanza kutafuna mifupa iliyomshinda fisi. Moja ya mfupa mgumu ni ule wa sensa ya watu na makazi. Waislamu walitaka kugomea sensa isiyo na kipengele cha dini. Jakaya akaongea na mashekhe, ngoma ikaisha, wakashikana mikono, wapenda amani tukagonga meza kwa utamu wa maridiano. Unajua Jakaya ni fundi sana wa kuongea, akifungua mdomo na lile tabasamu lake unaloweza kuchukulia mkopo, hata uwe umefura namna gani, utalainika mwenyewe. Ana kiswahili flani amazing. Utasikia ukitaka kula lazima uliwe!

Hata lilie sekeseke la nani achinje lilimalizwa kirahisi na wasaidizi wake. Mzee Pinda alisema jamani mbona miaka yote Waislamu ndo wamekuwa wakichinja? Basi utaratibu huo uendelee. Steven Masatu Wassira, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais enzi hizo naye akapigilia msumali. Waisilamu wakaachiwa mabucha,  wachonganishi wakanuna, sisi tukaendelea na ujenzi wanchi.

Nakumbuka wakati huo nikifundisha pale chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT Mwanza nilimualika Mzee Wassira kuongea na wanafunzi wangu wa Sociology kuhusu hizo vurugu za kuchinja. Wakati huo nikifundisha Conflict Resolution. Mjadala ulikuwa mtamu. Mezani tulikaa mimi, Wassira, Padri Charles Kitima na Profesa Adelardus Kirangi enzi hizo ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria. Leo Prof. Kirangi ndo Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Padri Kitima ni Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Tanzania na mimi ni mwandishi wa Historia za Viongozi, wote tukibeba fito kujenga nyumba moja kwa sababu Jakaya alisema tusigombanie fito kama tunajenga nyuma moja. Jakaya kwa maneno! Muhenga muhenga!

Aliponifurahisha sana ni jinsi alivyoushona ule  mpasuko wa Zanzibar uliomtoa jasho Mzee Mkapa. Tatizo la Mkapa ilikuwa mbabe, jamaa alikuwa na zero tolerance. Aliwahi kusema mtaji wa maskini ni nguvu zake, siyo akili. Jakaya akaumaliza kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Mwanasiasa Said Natepe, aliyepinga kwa uzoefu badala ya weledi akabaki solemba.

Mzee alitafuna mifupa mingi lakini wa ule wa katiba mpya ukamshinda. Tatizo aliuanza kwa kushindwa. Ni baada ya kuwateua mahasimu wake ndani na nje ya CCM kusimamia zoezi, wakamuwekea mtego akaukwepa. Nakumbuka alimteua Warioba kuwa Mwenyekiti, Joseph Butiku mjumbe, Prof. Mwesiga Baregu na hayati Dkt. Sengondo Mvungi. Kumbuka Warioba na Butiku walimsapoti Salim aliposimama na Jakaya, Jakaya akawashinda wakanuna, alipoingia Ikulu wakaanza kuvugumiza mawe Ikulu..

Jamaa wakaja na zengwe la serikali tatu na wakati kwa miaka 23 walivyokuwa na Mzee Nyerere hawakuwahi kufungua mdomo kutaka serikali tatu. Hata Rais Jumbe alipopeleka wazo la serikali tatu bungeni na kupokonywa urais hakuna aliyemtetea Jumbe. Kadhalika Jaji Francis Nyalali alipondekeza Muungano wa serikali tatu Nyerere akachomoa hakuna aliyefungua mdomo, sasa walitoa wapi ujasiri kipindi cha Jakaya? Jakaya akajua hili ni zengwe hili, hawa jamaa wanataka Muungano unifie. Hawanijui nini.

Jakaya akasema sikilizeni, serikali yangu haiwezi ruhusu serikali tatu, kwanza serikali tatu ni hatari, inaweza kupinduliwa na jeshi. UKAWA wakazila na kutoka Bungeni ili kuishitaki CCM kwa wananchi, wakapigwa pini, badala yake wakaishia kushambuliwa kwamba wamekula posho zote kususia bunge. UKAWA na la Profesa wao Ibrahimu Lipumba wakapoteana hadi leo hawajarudi.

Miaka kumi ya Jakaya katika kiti cha enzi ikafika mwisho, akamkabidhi kijiti Dr. John Pombe Magufuli wa Chato kuipeperusha bendera. Kampeni za Magufuli zikawa burudani tupu. Wakati CCM wakitukana upinzani, Magufuli aliitukana CCM kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Wafitini wakamfuata Jakaya ampige pini Magufuli kwa kuidhalilisha serikali yake majukwaani. Jakaya akawaambia sioni tatizo lolote wala sishangai kusikia mgombea huyo akiikosoa serikali yake kwa kuwa Tanzania inahitaji muelekeo mpya kwa sababu Jakaya hakuwa mtu wa kulipuka kama mapepo kwenye maombezi ya Gwajima. Magufuli alipoingia Ikulu wafitini wakasema tena Jakaya hachomoi. Jakaya akacheeekaaa, “ati sichomoi, kwani nimechomeka nini?” Baba Miraji bana!

Anakwambia yaliyofanyika katika utawala wake ni mengi na mengine hayajafanyika. Huwezi kufanya yote. Very logical. Hata hivyo mistake kubwa ya Jakaya ni upendo wa mshumaa kumulikia wenzake huku yeye akiteketea walisema wachambuzi. Ati alipanda kwenye meli na mizigo aliyojua kabisa itasababisha wazame lakini akashindwa kuitupa. Wengi walitamani awe mkali kama Nyerere. Jamani hivi Nyerere mnamjua nyie au mnaongea tu kwa sababu midomo ni mali yenu? Enzi za Nyerere ulijua kibarua kimeota kupitia taarifa ya habari ya saa 2:00 usiku ya Redio Tanzania Dar es Salaam tena ikisomwa na David Wakati! Mliofanya mitihani kwa kuandikiwa ubaoni na mwalimu mnanielewa.

Ukiachilia mbali upendo wake wa mshumaa, Jakaya alibarikiwa uvumilivu mkubwa katika medali za siasa ndo maana alipata tuzo nyingi kuliko marais wote Tanzania ukiachia Nyerere. Hata alipotukanwa na mtoto mdogo ati yeye ni dhaifu hakutia neno, lakini pia siku ile Mzee Magufuli alipofoka kuhusu bandari ya Bagamoyo ati ni mambo ya kipumbavu kabisa kusaini mikataba kama ile, Jakaya hakutia neno. Utamaduni wa viongozi wa Tanzania huwa naupenda sana, wakiishatoka madarakani wanakaa zao pembeni ili Rais afanye yake bila kubughuziwa kwa sababu wanajua ilivyorahisi kusema na ngumu kutenda. Ni Mzee Nyerere tu ndo alimpa wakati mgumu mzee Mwinyi. Mwinyi naye kwa wingi wa hekima alikaa zake kimya! Hakuwahi kumjibu Nyerere! Nakumbuka na Mkapa naye alipigwa mkwara na Nyerere. Alimwambia utabinafsisha hadi magereza wewe.

Halafu unaikumbuka ile filamu ya mapanki ilivyotaka kuimaliza serikali yake akashituka? Iliandaliwa na Hubert Sauper, raia wa Ufaransa. Inaitwa Darwin Nigtmare. Ilionyesha Tanzania kama takataka. Yaani madege yaliyoleta silaha Afrika yaliondoka na minofu ya samaki wetu na sisi kubaki na mapanki. Richard Mgamba wa The Gardian Tanzania alipata msukosuko kweli maana ndo alitoa tafsiri ya Kiingereza kwa ajili ya filamu hiyo. Salvatory Rweyemamu alutumia nguvu, akili na fedha za Ikulu kuubadilisha ukweli wa wasukuma kula mapanki waungwana tukashangaa na wale wengine wakapiga makofi.

Huyu Salvatory enzi za Gazeti la Rai ndo alikuwa mrusha mawe ikulu enzi za Mkapa lakini enzi za Kikwete akawa mpangua mawe yaliyorushwa Ikulu kwa sababu pesa haidanganyi. Salva alitetea hadi utabiri wa Sheikh Yahaya aliposema mtu  atakayejitokeza kumpinga Rais Kikwete katika uchaguzi wa 2010, atakufa, baada ya uchaguzi, mtabiri akafa yeye kwa sababu Mungu hapangiwi. 

Rweyemamu pamoja na juhudi zake za kupangua makombora Ikulu hakuamini macho yake serikali ikiangushwa kwa kashfa ya Richmond. Waziri mkuu Edward Lowassa alijiuzulu; baraza la mawaziri likavunjika, Mizengo Pinda akawa waziri mkuu. Hii inaitwa kufa kufaana. Lowassa akawabariki upinzani cha kusema, wakamsema kweli. Halafu Mungu alivyo wa ajabu haohao walimchafua Lowassa ndani na nje ya nchi ndo walikuja kumsafisha wenyewe. Ni baada ya Lowassa kukatwa CCM na wao kumpokea, wakamsame na kumuondolea dhambi zake zote kisha wakamvisha taji la kupeperusha bendera ya Urais kwa jina la UKAWA. Lowassa alivyoukosa Ukulu aliamua kurudi zake nyumbani CCM kwa sababu ng’ombe akivunjika mguu hurudi zizidi. 

Majanga yalikuwa mengi labda ndo maana Jakaya alichagua kuishi maisha ya kelele za mlango hazinizuii kulala, macho ya mbwa hayanizuii kula nyama. Maana akigeuka kule EPA, akirudi huku Muungano, akiinama Richmond, akiinuka uchinjaji, akijinyosha katiba, akinywa maji anaona mahakama ya kadhi kama mpenzi wako anavyokudanganya ati akinywa maji anakuona wewe ili akuibie hela. Waislamu walipombana kwenye mahakama ya Kadhi, Mchungaji Christopher Mtikila alijitokeza kuwapinga Waislamu, akidai kwamba madai yao ni kinyume cha katiba.

Mtikila alibarikiwa akili ya kusumbua wenzake! Kuna siku Mtikila alimshitaki Askofu Mkuu wa Anglikana Dk. Valentino Mokiwa kwa kumshika makalio. Mtikila anasema Askofu alimuita kujadili tamko la Mtikila kwamba Kanisa la linajihusisha na ufisadi, ukiwemo wizi wa vifaa vya Hospitali ya Mission ya Millo iliyoko Ludewa Njombe. Mtikila alifika na wenzake watatu na muda mfupi Askofu alisimama na kuwataka wajumbe wote wakaguliwe kama kuna mtu ana kinasa sauti. Askofu naye alisimama na kuungana na wenzie kuwapekua kina Mtikila.

Katika upekuzi ule Mtikila akasema Askofu alianza kupenyeza mikono yake kwenye shingo kuelekea chini kisha huko chini mikono ya Askofu ilionekana waziwazi ikipapasa makalio ya Mtikila. Mtikila aliiomba Mahakama imwamuru Askofu alipe fidia ya shilingi bilioni moja kwa kumsababishia mfadhaiko, masikitiko, wasiwasi, aibu katika jamii na kupata shinikizao la damu la mara kwa mara na matatizo ya moyo kila anapokumbuka kitendo hicho. Ukitaka kujua walimalizaje katafute mwenyewe sitaki umbea mimi!

Nimalizie kwa kusema kwamba, Jakaya ni mume wa Salma na baba wa  Ridhiwani, Salama, Miraj, Ally, Khalifa, MwanaAsha, Khalfan, Rashid na Mohamed. Mohamed ni mtoto wa kuasili. Ridhiwani na mama yake ni wabunge. Ridhiwani alizaliwa Aprili 16, 1979 baba akiwa vitani Uganda. Nasikia Jakaya na Kagame walikukuwa kikosi kimoja wakazinguana kiana huko misituni ndo maana hadi leo haziivi. Kwahiyo siku ile Jakaya ashauri Kagame akae na mahasimu wake wa Rwanda na Congo wayamalize, Kagame akamind,lilikuwa ni bifu la toka vitani Uganda.

Kutokana na Jakaya,nimejifunza mambo mengi, lakini kutokana na muda chukua haya matano!

Moja; maisha ni mzunguko, zunguka nayo bila kumnyanyasa aliyechini yako, maana hujui kesho atakuwa nani. Pius Msekwa alikuwa bosi wa Kikwete na baadaye Kikwete akawa bosi wa Msekwa!

Mbili, wanapokurushia mawe yakusanye ujenge ghorofa kwa sababu kisichokuua kinakuimarisha. Kikwete alivunja rekodi katika kupondwa akaishia kusema mtanikumbuka.

Tatu: Mtumikie kafiri utimize uachokitafuta. Jakaya alinunuliwa viatu kwa mara ya kwanza alipotoka jandoni, kwenda navyo shuleni, mwalimu akampiga marufuku kurudi shule tena na viatu ati kwa sababu wanafunzi wengine hawana na yeye akatii.

Nne: Dhamana ya uongozi haikufanyi uwe ni mtu zaidi ya watu wengine, haikufanyi uwe na haki kuliko wengine kwa sababu maisha ni kutegemeana.Hili ni funzo kwa wale wanaotumia vyeo vyao kuwaweka ndani wenzao. Kuna kiongozi aliwahi amuru kijiji kizima kiwekwe ndani.

Tano: Mawazo hayapigwi rungu, mawazo yanashindwa na mawazo yaliyo bora zaidi. Hoja zinapotolewa  zinahitaji majibu ya kueleweka, sio kutumia vitisho kuzima hoja ambazo wananchi wanahitaji majibu.

Huyu ndo Jakaya Mrisho Kikwete, rais pekee Tanzania mwenye majina pure ya kiafrika, hana majina ya kizungu! Ipo neema katika majina ya nyumbani, ipo balaa katika kurithi majina usiyoyajua! Wengi tuko mtegoni!

Wasalam Aleykum!

Friday, May 1, 2020

TANZIA

Je wajua kuwa Augustine Mahiga ni mmoja kati ya wanadiplomasia watatu wabobezi nchini?
Waliobaki ni Membe na JK
Tutakukumbuka daima

HISTORIA YA LUGHA Nadharia juu ya lugha ya kiswahili Kuna nadharia mbali mbali zinazoelezea asili ya lugha ya ...