Friday, February 15, 2019

TUNGO

Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. Au tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.

Kwa maana hii, tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kunda kishazi na kishazi kuunda sentensi. Kama tulivyokwisha kuona hapo juu tungo huanzia neno; rejea aina za tungo.

Aina za tungo

Bainisha aina mbalimbali za tungo

Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu. Mfano; anacheza, kakimbia.

Tungo Kirai: ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu. Mfano; mtoto mzuri, kiyama chake, bondeni

Tungo kishazi:Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.

Kirai na Uainishaji wake

Maana ya Kirai na Uainishaji wake

Dhana ya kirai itaeleweka vizuri kwa kuzingatia sifa zake zifuatazo:

Kirai huwa ni kipashio cha kimuundo kisichokamilika; yaani ni kipashio kisichokuwa na muundo wa kiima – kiarifu kama zilivyo sentensi ambazo zinahusisha mtendaji wa tendo na tendo linalotendwa.Kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu la kirai husika.Kirai ni tungo, yaani ni aina moja wapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno,kishazi na sentensi.Kirai hudokeza maana, lakini maana hiyo si kamili.Maneno katika kirai lazima yapangwe kimantiki kwa mpangilio unaokubalika katika sarufi ya lugha husika. Japo virai huainishwa kimuundo, huweza kutumika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi. Kirai huweza kutokea upande wowote, wa kiima au kiarifu katika sentensi. Kirai ni kikubwa kuliko neno

Kama tulivyobainisha hapo juu aina ya virai hukitwa katika aina za maneno ambazo ndizo chimbuko la mahusiano maalumu ndani ya vipashio hivyo.

Kirai nomino (KN);Ni kirai ambapo neno lake kuu ni nomino. Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino au mahusiano ya nomino na neno au mafungu ya maneno.Kirai kitenzi (KT); Kirai-kitenzi ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi au katika mahusiano ya Kitenzi na neno au mafungu mengine ya maneno. Hii ina maana kuwa neno kuu katika aina hii ya virai huwa ni kitenzi.Kirai kivumishi (KV); Kirai-kivumishi ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika kivumishi. Kwa kawaida muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno au fungu la maneno linaloandamana nacho.Kirai Kielezi (KE); Tofauti na aina nyingine ya virai miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo.Virai viunganishi (KV); Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya kwa na katika, au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno mengine kirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kiunganishi.

Tungo kishazi

Maana ya Kishazi na Uainishaji wake

Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.

Sifa za kishazi

Kishazi hupatikana katika/ ndani ya sentensi.Lazima kishazi kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.Baadhi ya vishazi haviwezi kujitegemea kama sentensi ikiwa vitaondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu.Vishazi vingi, hata vishazi huru huwa na kiima dhahiri.Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru huwa na kitenzi kimoja kikuu.Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.Kishazi hutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi.Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana.Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, Lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja.

Aina za vishazi

Vishazi huru: Kishazi huru ni kishazi kinachotaewaliwa ka kitenzi kikuu, ambacho kwa kawaida hutoa ujumbe kamili usiohitaji maelezo zaidi ya kukamilisha maana. Ni kishazi ambacho hata kikiondolewa katika muktadha wa sentensi ambamo vimejikita huweza kujitegemea kama sentensi.Vishazi tegemezi: Kishazi huru ni kishazi kinachotawaliwa ka kitenzi kisaidizi, ambacho muundo wake hukifanya kutegemea kitenzi cha kishazi huru ili kuweza kutoa ujumbe uliokusudiwa. Kishazi tegemezi peke yake hakitoi ujumbe unaojitosheleza

Sifa za Kishazi tegemezi

Kishazi tegegemezi hutoa maana kamili kinapoandamana na kishazi huru.Kishazi tegemezi kinaweza kufutwa katika sentensi bila kuharibu maana ya sentensi nzima.Kishazi tegemezi hutambulishwa na viambishi vya utegemeziVinavyoambatanishwa kwenye kitenzi.Kishazi tegemezi vile vile kinaweza kutambuliwa kwa kuwepo vishazi kama vile ingawa, kwamba, ili, kwa sababu, mzizi wa amba, mofu ya masharti n.k

Aina ya vishazi tegemezi

Vishazi tegemezi vivumishi

Vishazi tegemezi vinavyotokea pamoja na nomino inayovumishwa.Vishazi tegemezi visivyoambatana na nomino inayovumishwa

Vishazi tegemezi vielezi

Vishazi tegemezi vya mahaliVishazi tegemezi vya wakatiVishazi tegemezi vya namna au jinsiVishazi tegemezi vya mashartiVishazi tegemezi vya hali, hitilafu au kasoro iliyoko katika tendo.Vishazi tegemezi vya sababu/chanzo

Dhima na hadhi ya vishazi

Kishazi chaweza kuwa huru kikajitegemea chenyewe kwa kuwa na maana kamili inayojitosheleza. Lakini kuna vishazi ambavyo havijitoshelezi vyenyewe, bali hutegemea vishazi vingine. Kishazi huru kina hadhi ya sentensi (sahili). Kishazi tegemezi hakina hadhi hii, vishazi tegemezi ambavyo hutegemea vishazi vingine hushuka daraja na kuchukua dhima ya kikundi. Baadhi ya vishazi tegemezi huchukua dhima (hufanya kazi) ya kivumishi katika tungo ambayo kwa kawaida ni dhima ya kikundi au neno. Vishazi hivi huvumisha nomino katika tungo hiyo

Sentensi

Maana ya sentensi

Sentensi ni kifungu cha maneno kuanzia neno moja na kuendelea chenye muundo wa kiima na kiarifu na kinacholeta maana kamili.

Sifa za sentensi

Sentensi lazima iwe na mpangilio wa maneno ambao unakubalika na wazungumzaji wa lugha husika.

Sentensi lazima ikamilike kimaana, kimuundo na kisarufi.Sentensi huwa na muundo wa kiima na kiarifu /huwa na kirai nomino na kirai kitenzi.Sentensi huweza kuwa na zaidi ya kiima kimoja na kiarifu zaidi ya kimoja.Sentensi inaweza kuundwa na kitenzi kikuu kimoja au zaidi.Sentensi inaweza kuundwa na kishazi huru kimoja au zaidi na kishazi tegemezi kimoja au zaidi.Sentensi huonyesha hali mbalimbali, kama vile amri, ombi, mshangao, swali n.k

Muundo wa sentensi

Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima

Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima unakuwa na vipengele vifuatavyo:

Kiima:Ni sehemu katika sentensi ambayo hujaza sehemu ya mtenda au mtendwa wa jambo linaloelezwa. Katika tungo kiima hutokea kushoto mwa kitenzi.Kiarifu:Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayo arifu tendo lilofanywa, linapofanywa au litakapofanywa. Kiarifu ndiyo sehemu muhimu zaidi katika sentensi ambayo wakati mwengine huweza kusimama pekee, kwani wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima.

Vipashio vya kiima

Nomino peke yakeNomino, kiunganishi na nominoNomino na kivumishiKivumishi na nominoKiwakilishi peke yakeKiwakilishi na kivumishiNomino na kishazi tegemezi vumishiKitenzi jinaNomino na vivumishi zaidi ya kimojaKitenzi jina na nominoUmbo kapa

Taarifa zitolewazo na kiarifu kuhusu kiima

Kiima ni naniKiima kina niniKiima hufanya niniKiima kinahisi nini

Sifa za kiarifu

Huwa na kitenzi na pengine huambatana na maneno mengine.Kiarifu kwa kawaida huja baada ya kiima

Vipashio vya kiarifu

Kitenzi kikuu peke yake.Kitenzi kisaidizi au vitenzi visaidizi vilivyosambamba na kitenzi kikuu.Kitenzi kishirikishi na kijalizoYambwa (shamirisho)KijazalioChagizo

Sifa za chagizo

Chagizo kwa kawaida huwa ni kielezi au kirai husishi ambacho kinafanya kazi kama kielezi.Kwa kawaida ni vipashio vya ziada. Si lazima viwepo katika sentensi ili ijisimamie.Huwa cha lazima ikiwa kinafuata kitenzi kishiriki. Hali ikiwa hivyo, kinafnaya kazi kama kijalizo.Hutumika kufafanua kitenzi/kivumishi /kielezi.Hutumika kujaliza kiima/kama kijalizo.

Aina za sentensi

Uainishaji wa sentensi

Aina za sentensi kimuundo ni pamoja na hzi zifuatazo

Sentensi sahili

Ni sentensi ambayo huundwa na kishazi huru kimoja. Sentensi ya aina hii huwa inaelezea taarifa moja tu. Mfano; Wanafuzi wanafanya mtihani; Walinzi walitaka kunizuia nisiingiendani.

Miundo ya sentensi sahili

Muundo wa kitenzi kikuu peke yake. Mfano: Gari limeangukaMuundo wa kitenzi kikuu na kitenzi kisaidizi. Mfano:Mgosiyuda alitaka (TS) nisipate (T) utajiriMuundo wa vira-vitenzi vilivyokitwa katika kitenzi ‘kuwa’. Mfano: Johnamekuwa akiangaliaTV kwa muda mrefu sana.Muundo wa kitenzi shirikishi. Mfano: Kiswahili ni tunu ya Taifa

Sifa za sentensi sahili

Ina kiima ambacho kimetajwa wazi au kimeachwa kutajwa kwa kuwa kinaeleweka.Ina kiarifu ambacho kimeundwa na kitenzi kikuu kimoja au kitenzi kikuu na kitenzi kisaidizi au kitenzi kishirikishi na kijalizo na chagizo.Haifungamani na sentensi nyingine na hivi inajitosheleza kimuundo na kimaana.

Sentensi changamano

Hii ni sentensi yenye kishazi huru kimoja au zaidi na kishazi tegemezi kimoja au zaidi. Sifa moja kubwa ya sentensi changamano ni kuwa na kishazi tegemezi ambacho hutegemea kishazi kingine huru ndani ya sentensi hiyo. Msingi muhimu wa uhusiano ndani ya sentensi hizo ni ule wa kishazi kimoja kutegemea kingine

Sentensi changamano ina muundo wenye vishazi virejeshi. Mfano: Gari liliopinduka jana jioni halikuharibika hatata kidogo.

Sentensi ambatano

Hii ni sentensi inayojengwa na sentensi mbili au zaidi zilizounganishwa kwa kutumia viunganishi kama vile likini, wala, au, na, nakadhalika.

Miundo ya sentensi ambatano

Miundo yenye sentensi sahili tu. Mfano: Mwalimu anafundisha wakati wanafunzi wanapiga kelele.Miundo yenye sentensi sahili na changamano. Mfano: Walinzi waliposhindwa polisi waliwasaidia lakini hawakuweza kuwakamata majambazi.Miundo yenye sentensi changamano tu. Mfano: Barabara zilizojengwa na wakoloni zimedumu hadi leo wakati zile zilizojengwa na Wachina hata mwezi hazifikishi.Miundo yenye vishazi visivyounganishwa kwa viunganishi

SARUFI

DHANA YA SARUFI

Sarufi ni taaluma ya lugha inayochunguza na kuchanganua vipashio na kanuni mbalimbali zinazotawala muundo wa lugha,

Matinde, (2012)
Sarufi ni utaratibu wa kanuni ambazo humwezesha mtumiaji wa lugha kutunga tungo sahihi zinazoeleweka mara zinapotamkwa. Kapinga, (1983). Dhana ya sarufi inatafsiriwa katika mitazamo tofauti lakini yenye kuhusiana. Mtazamo wa kwanza tunaweza kusema Sarufi ni taaluma ya uchambuzi walugha inayojumuisha viwango vyote vya uchambnuzi yaani kiwango cha umbo sauti (fonolojia), kiwango cha umbo neno (fonolojia), kiwango cha miundo maneno (sintaksia) na kiwango cha umbo maana(semantiki), (Massamba, 1999).                                            

DHANA YA SARUFI MUUNDO VIRAI Sarufi muundo virai ni mkabala wa kimapokeo ambao haujihusishi na sarufi miundo katika marefu na mapana yake, ambapo zilijihusisha sana na sentensi sahili,

(Massamba 1999). Sarufi muundo virai ni kitengo cha sarufi geuza maumbo zalishi, ambacho hujikita katika matumizi ya sheria chache kuzalisha sentensi nyingi zisizo na kikomo, ambazo zina usarufi na hata zile ambazo hazijawahi kutungwa,

( Matinde, 2012). Sarufi muundo virai ni mpangilio wa vitu vidogo vilivyowekwa pamoja na kujenga kitu kikubwa zaidi. Sarufi miundo virai ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai vinayoiunda na kasha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neno mojamoja lililokiunda kirai, (Massamba, 2001).

 DHANA YA SARUFI GEUZI

Ugeuzi ni utaratibu unaotumiwa kubadili umbo la tungo kuwa umbo jingine kwa kutumia kanuni maalumu. Kwa hiyo ugeuzaji ni mbinu ya kisarufi ambayo hutumiwa katika sarufi geuza maumbo zalishi kuzalisha sentensi lukuki kwa kufuata sheria mahususi,

(Matinde, 2012). Sarufi geuzi hueleza ujuzi wa lugha ambao msemaji mzawa anao ujuzi anaomwezesha kutumia lugha

(Habwe na Karanja,2007). Sarufi geuzi maumbo ni utaratibu wa kubadili maumbo kuwa maumbo meng kwa kufuata kanuni maalumu

(Matinde,2012). Zifuatazo ni tofauti kati ya sarufi miundo virai na sarufi geuzi: Hutofautiana katika lengo. Lengo laohalifahamiki zaidi ya kutumia taratibu za kijarabati zinazohusu ukusanyaji wa data na kuzichambua pamoja na kuunda kanuni kwa kutumia data hizo.

Lakini, Lengo la sarufi geuzi liko bayana, hujitokeza dhahiri. Lengo la sarufi hii ni kufafanua umilisi wa ujuzilugha ambao huwa mwanalugha anao. Umilisi huo humfanya mwanalugha kutambua viambajengo kati ka tungo, katika mtazamo wa ndani yaani muundo wa ndani. Hutofautiana katika miundo.

Sarufi miundo virai, hii huwa inajikita katika miundo ya nje, ambayo huchunguza na kuchambua sentensi katika umbo la nje. Mfano; Mama anakula ugali Hivyo huonyesha tu aina ya maneno husika katika sentensi au tungo kama vile: Mama- Nomino, Anakula- Kitenzi, na Ugali- Nomino. Ilihali, Sarufi geuzi, hii huwa imejikita katika kuchungaza sentensi kama umbo la ndani na umbo la nje. Muundo wa ndani ni uchopekwaji katika miundo hiyo ambapo muundo wan je lazima upitie katika muundo wa mofofonemiki na kuweka katika kitengo cha fonolojia. Hutofautiana katika vitengo.

Sarufi geuzi ni sarufi ambayo inafumbata vitengo vyote vya lugha ambavyo ni fonolojia, sintaksia, semantiki, na mofofonemiki ambapo kitengo cha fonolojia hushughulikia sauti za lugha, kitengo cha kisintaksia hushughulika na uundaji wa sentensi, kitengo cha semantiki hushughulika na ufasili wa maana, na kitengo cha mofofonemiki huwa na kazi ya kuibadili njeo za wakati. Ilihali Sarufi miundo virai hufumbata kitengo cha mofolojia ambapo sentensi iligawanywa katika kiunzi cha aina za maneno kama Nomino, Kitenzi, Kivumishi, Kielezi na kihunzi hicho kilijulikana kama utaratibu wa uchanganuzi wa viambajengo. Hutofautiana katika uhusiano wa sentensi. Sarufi geuzi ilipiga hatua kubwa, kwanza huonyesha uhusiano uliopo kati ya maumbo mbalimbli ya sentensi au tungo.

Na pia kuonyesha uhusiano unaoweza kuwepo baina ya sentensi moja na sentensi nyingine. Mfano: (1) Mtoto mrefu anacheza, na si kusema kuwa Mtoto anacheza mrefu Huu ni uhusianao kati ya maumbo. Mfano: (2) Juma alipiga mpira Mpira ulipigwa na Juma Huu ni uhusiano wa sentensi moja na sentensi nyingine. Ilihali Sarufi miundo virai haionyeshi uhusiano kati ya sentensi moja na sentensi nyingine. Hutofautiana katika uwazi. Sarufi geuzi huonesha sentensi sahihi na ambazo sio sahihi pia huonesha sentensi ambazo zinakubalika na sentensi zisizokubalika kwa msemaji mzawa. Ilihali Sarufi miundo virai yenyewe haina uwazi huo. Hitimisho ni kwamba, Sarufi geuzi ilianzishwa kutokana na mapungufu katika sarufi muundo virai. Sarufi iliyokuwepo, sarufi miundo virai, ilishindwa kuonyesha mahusiano yaliyokuwepo baina ya sentinsi zinazo husiana kimaana. Hivyo kutokana na upungufu huo kulikuwa na haja ya kuonyesha uhusiano huo. 

                 
                 MAREJELEO

Kapinga,M.C.(1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Dar-es-Salaam: TUKI. Massamba, D.T., Kihore,M.Y.& Hokororo.(1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). Dar-es-Salaam: TUKI. Matinde,S.R.(2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD

KAMUSI


WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

CHUO CHA UALIMU CHA MT. MAURUS

MADA NDOGO :KAMUSI YA LUGHA 

MWALIMU WA SOMO:LAMECK

MASWALI 

Nini maana ya kamusi? 

Umuhimu wa kamusi 

Mambo ya kuzingatia katika kamusi 

Sifa za kamusi kubwa na kamusi ndogo 

WASHIRIKI 

Masal Masal 

James Kalua 

KAMUSI YA LUGHA; MAANA, AINA, TAARIFA NA DHIMA ZAKE.

MAANA YA KAMUSI

Massamba (2012:24) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno katika lugha, yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana au fasili zake; katika uchanganuzi wa lugha haya ni maneno ya kileksika, yaani yasiyokuwa ya kisarufi au kifonolija.

Tuki (1990:21) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana na fasili zake.

Wamitila (2003:76) kamusi ni kitabu ambacho kina orodha ya maneno katika lugha Fulani ana ambayo hupangwa ki-abjadi au kialfabeti. Maneno haya huelezewa maana zake mbalimbali na labda hata vyanzo vyake.

Matinde (2012:273) kamusi ni kitabu chenye mkusanyiko wa maneno sanifu katika lugha mahususi yaliyoorodheshwa kialfabeti na kutoa taarifa za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, na hata kisemantiki.

Nyambari na Masebo (2012:179) kamusi ni kitabu cha marejeleo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani, na kupangwa kwa utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo msomsji huweza kuelewa.

Kwa ujumla  kamusi ni kitabu chenye orodha ya maneno mbalimbali yaliyopangwa vizuri kwa kufuata alfabeti na hutoa taarifa mbalimbali kama vile maana, matamshi n.k.

MUUNDO WA KAMUSI

i)  Utangulizi wa Kamusi

Hii ni sehemu ya mwanzo ambayo hutangulia matini yenyewe ya kamusi.

ii)  Matini ya Kamusi

Hii ni sehemu ambayo inaonyesha vidahizo na fahiwa zake kuanzia herufi A-Z.

iii)  Sherehe ya Kamusi

hizi ni baadhi ya taarifa ambazo huwa zimeandikwa mwishoni mwa kamusi. Kwa mfano majina ya nchi, lugha za mataifa duniani, vipimo vya urefu, vipimo vya uzito, ujazo  n.k.

AINA ZA KAMUSI

Kwa kutumia kigezo cha LUGHA kuna aina kuu tatu (3) za kamusi

i) kamusi wahidiya

hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha moja

ii) kamusi thaniya

Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha mbili.

iii) kamusi mahuluti

Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha zaidi ya mbili. Kwa mfano Kiswahili-kiingereza-kifaransa.

KWA KUTUMIA KIGEZO CHA UKUBWA

Zipo aina tatu za kamusi kwa kutumia kigezo hiki cha ukubwa kama ifuatavyo 

(i)Kamusi ndogo-hii ni kamusi ambayo huwa na maneno yasiyozidi 10,000 

(iiKamusi ya kati - hii ni kamusi ambayo huwa na maneno yasiyozidi 25,000

(iii)Kamusi kubwa- hii ni kamusi ambayo huwa na maneno zaidi ya 50,000 

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA KAMUSI

Kulingana na Newell (1995) amebainisha nduni zifuatazo za Kongoo

a.       Maumbo yasiyo na mnyambuo ambayo hutokea katika hali ya Kifonolojia (Matamshi) ndiyo huingizwa katika kamusi mfano; mama, shangazi, sana, suri n.k

b.    Maneno ambayo hayana viambishi ndiyo hudondolewa katika kamusi mfano; adhimisha, piga, adhimu vinaweza kuwa kidahizo.

c.       Maumbo huru yenye sifa za kifofonemiki huweza kuorodheshwa kama kidahizo. Umbo lenye mkazo mmoja tu.

d.      Maumbo yanayotambuliwa na wazungumzaji asilia wa lugha hiyo kama neno, yanaweza pia kuingizwa katika kamusi kama kidahizo. Hapa ni muhimu kupata tajiriba kutoka kutoka kwa wazawa.

e. Maumbo ambayo ni rahisi kuyabainisha kama neno yanapokuwa katika sentensi, huingizwa katika kamusi kama kidahizo:Kijana mdogo sana amesafiri leo asubuhi kwa ndege ya fastjet

f.      Maumbo yanayotokea mara kwa mara mfano mtoto Vs Kitoto hutumika mara kwa mara katika maandishi na mazungumzo. Katika kongoo ya Kiswahili kuna maneno yapatayo milioni kumi (10,000,000/=).

g. Maumbo yote yale yanayowakilisha maana ya msingi (Basic meaning) ya leksimu huingizwa katika kamusi kama kidahizo mf. Askarikanzu, mpigambizi, amevaa miwani n.k

h. Maumbo ya mashina ambayo maneno nyambulishi mengine yanaweza kuundwa, yanaweza kuorodheshwa pia kama kidahizo

i.       Maumbo yanayoweza kutumika kupata vitomeo vidogo (sub-entry) yanaweza kuingizwa katika kamusi kama kidahizo.


Mambo ya kuzingatia katika Uteuzi wa Vidahizo vya kamusi

1.      Umbo la neno: ni lile umbo ambalo mtumiaji wa kamusi anatarajiwa kulitafuta, mfano: pig.a, stahimili, dada, askari (askarikanzu).

2.      Muundo wa neno: neno linaweza kuundwa na:

-         Mofimu huru moja mf. Kalamu, Nyoka, Baba na mama

-      Mofimu zaidi ya moja kwa pamoja mf. Mchezaji (m-chez-a-ji), mkulima (m-ku-lim-a) n.k

-      Maneno mawili au zaidi ambayo yameambatana na kuwa na maana moja mf. Kifungua kinywa (kifunguakinywa), mwana mapinduzi (mwanamapinduzi), askari kanzu (askarikanzu).

-         Nahau, nahau ina hadhi ya neno kwa hiyo nayo inaingizwa katika kamusi kama kidahizo mf. Piga maji, vaa miwani, zunguka mbuyu.

3.     Uingizaji wa viambishi:wasomaji wa kamusi hawatafuti viambishi, hata hivyo husaidia kuelewa maana zalishwa. Vioneshwe mbele ya shina la neno husika kwa kutenganishwa na alama ya mawimbi. Mf. To.a ~ le, ~lew,~an, ~lesh n.k

4.   Tahajia: ni muhimu kufanya uamuzi wa tahajia itakayotumika kwa maneno yenye tahajia zaidi ya moja, kwa mf. Tasinifu Vs Tasnifu, Theatre Vs Theater, Burangeti Vs Blanketi, Kula Vs Kura

5.  Majina ya Pekee: majina ya pekee huwa hayaingizwi katika kamusi kama kidahizo isipokuwa kwa yale ambaya yanahusishwa na uvumbuzi au mwanafalsafa fulani mf. Umaksi, Kanuni ya Newton. Maneno haya lazima yaingizwe katika kamusi kama kidahizo kutokana na sifa za ziadi yaliyonazo yanaondoka kuwa majina ya pekee tu.

6.    Uingizaji wa Maneno ya Mkopo: tahajia ya maneno ya mkopo iingizwe kwa kufuata tahajia ya lugha lengwa. Mfano Editor – Edita – Editori, radio- redio- radio, machine-mashini – mashine. Baada ya kuwa mtunga kamusi umeamua ni tahajia ipi itatumika, chagua moja na itumike kwa kamusi nzima.


Taaarifa zinazopatikana katika kamusi

Taarifa hizi huweza kuwa za kisarufi au kileksika

a) taarifa za kisarufi zinazoingizwa katika kamusi.

Nyambari na Masebo (2012:184) wameainisha taarifa zifutazo za kisarufi zinazopatikana katika kamusi.

·       Wingi wa nomino

·       Kategoria ya kisarufi ya kidahizo mf. Kitenzi (kt), nomino (nm) n.k

·       Vinyumbuo vya vitenzi mf. Piga-pigwa-pigana-pigika n.k

·       Ngeli za nomino mf. Mtu (A-YU), kazi (i-)

·       Matamshi ya neno

·       Elekezi au sielekezi. Mfano: Apiza kt [ele], Anguka kt  [sie]

·       Mifano ya matumizi

b) Taarifa za kileksia zinazopatikana katika kamusi

Matinde (2012:275-281) anaeleza taarifa zifuatazo za kileksia ambazo zinapatikana katika kamusi ya lugha.

·       Mpangilio wa vidahizo

·       Kategoria za maneno

·       Umoja na wingi

·       Upatanisho wa kisarufi

·       Uelekezi wa vitenzi

·       Maana ya vidahizo

·       Tahajia za maneno

·       Mifano ya matumizi

·       Methali, nahau na misemo

·       Timolojia ya leksimu

·       Michoro/ picha

·       Matamshi

DHIMA ZA KAMUSI

·       Huonesha tahajia sahihi za maneno

·       Huonesha maana za maneno

·       Huonesha matamshi sahihi ya maneno

·       Huonesha asili ya neno

·       Humsaidia mtumiaji kujifunza lugha za kigeni

·       Huonesha alama na vifupisho mbalimbali katika lugha husika.

                     Marejeleo

Massamba. D.P.B.(2004 ). Kamusi ya isimu na falsafa ya lugha. Dares salaam: TUKI

Masebo . J. A. & Nyangwine. N. (2012). Kiswahili kidato cha tatu na nne . Dares salaam: nyambari nyangwine publishers

Matinde. R. S. (2012). Dafina ya lugha. Isimu na nadharia. Kwa sekondari, vyuo va kati na vyuo vikuu. Mwanza : Serengeti bookshop.

TUKI (1990).kamusi sanifu ya isimu na lugha. Dares salaam: Tuki na Educational publishers and distributors ltd.

Wamitila. K. W. (2003). Kamusi ya fasihi, istilahi na nadharia. Nairobi: Focus publishers ltd

Chomboz.blogspot.com(25/11/2018 16:20).Mambo ya kuzingatia katika kamusi 

http://swa.gafkosoft.com(25/11/2018,16:21). Aina za kamusi 

HISTORIA YA LUGHA Nadharia juu ya lugha ya kiswahili Kuna nadharia mbali mbali zinazoelezea asili ya lugha ya ...